Anaitwa Eva Charles Kalunde ni mzaliwa wa Tabora.Ni lulu mpya kwenye tasnia ya muziki was Injili. Mbio zake za usanii zilianza kukomaa alipokuwa sekondari. Wakati huo akiwa anasoma shule ya sekondari Mwinyi iliyopo Tabora mjini. Alianza kujulikana kwa kuimba kwenye makutano ya wanafunzi maarufu kama "joint mass" zinazowakutanisha wanafunzi wa shule mbalimbali za Tabora. Hapo ndipo alipokutana na wanafunzi wenzake Mariam Joseph Kariuk na Martha Tiluli ambapo kwa pamoja waliamua kuanzisha band iliyojulikana kama Doxa Band.
Baada ya kuanzisha band hiyo ndipo walipoamua kumtafuta mlezi ambapo kwa pamoja waliamua kujiunga na kanisa TAG Maranatha Miracle Centre lililopo Cheyo B Tabora mjini chini ya Mchungaji Lutengano Mwasongela ambaye aliamua kuubeba mzigo huo na kuwa mlezi wao.
Eva Charles ni almasi iliyojificha kwa sababu si kitu cha kawaida kwa mtu mwenye kipaji cha kweli kama cha Eva kutovuma angalau tu kwa mkoa wa Tabora. Mara ya kwanza nilipomuona akiimba pamoja na band yao katika kanisa a TAG Maranatha Miracle Centre haikuwa rahisi kuamini kwamba nyimbo walizokua wanaimba ilikuwa ni live band. Kwani waliimba nyimbo zao kwa ustadi mkubwa kana kwamba walikuwa wanatumia back up CD. Na haikuwa rahisi kuamini kwamba hawakuwahi kurekodi hata albamu moja.
Eva Charles kwa sasa amemaliza kidato cha sita katika shule ya sekondari Uyui iliyopo pia Tabora mjini. Ndoto zake kimaisha ni siku moja kuwa msanii wa kimataifa wa muziki wa Injili na kuwa msomi mkubwa. Ili kutimiza hilo kwa sasa anatarajia kujiunga na chuo kikuu kwa mwaka wa masomo 2011/2012 kwa ajili ya kuitafuta shahada yake ya kwanza.